
Jamii ya wafugaji wa kijiji cha Terrat, Wilaya ya Simanjiro, inakumbushwa kutumia vizuri msimu huu wa mvua kuandaa malisho kwa ajili ya mifugo ili kuepuka hasara katika kipindi kijacho cha kiangazi.
Mwaka uliopita wafugaji wengi walipoteza mifugo yao huku wengine wakitumia gharama kubwa kunusuru mifugo kutokana na ukosefu wa malisho na maji. Mfugaji Daniel Leboi Ngoira anakumbusha uzoefu wake akisema:
“Ilinilazimu kutumia gharama kubwa kuhamisha mifugo, kukodi trekta na boza kwa ajili ya maji, na kununua chakula cha mifugo badala ya kutumia fedha hizo kununulia chakula cha familia. Tusipojiandaa mapema, tutaingia tena gharama hizi kubwa.”
Aidha, Mwenyekiti wa kijiji cha Terrat, Kone P. Medukenya, anawakumbusha wakazi wa kijiji hicho kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi, kulinda maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya malisho, na kushiriki kikamilifu katika mashamba darasa ya malisho yanayosimamiwa kwa ushirikiano na shirika la TNC kupitia mradi wa Green Kilimo.
“Huu ndiyo wakati wa kuhakikisha maeneo yetu ya malisho yanalindwa, kuhifadhi mbegu za majani, na kuhakikisha tunafuata utaratibu wa kulisha mifugo ili kipindi cha ukame kisitukute hatuna maandalizi,” amesema Medukenya.
Kumbukeni, maandalizi ya sasa yatasaidia kupunguza athari za ukame na hasara kwa mifugo yenu msimu ujao wa kiangazi.