![Wauzaji wa mahindi](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/bei-ya-mahindi.jpg)
Wakaazi wa kijiji cha Terrat wilaya ya Simanjiro wamelalamikia hali ya mfumuko wa bei ya mahindi ulivyongezeka kwa zaidi kutoka shilingi elfu 7,000 hadi shilingi elfu 15,000.
Jamii ya wafugaji wa kijiji cha Terrat, wilayani Simanjiro, mkoa wa Manyara, wanakabiliana na changamoto kubwa kutokana na kupanda kwa bei ya mahindi sokoni. Mahindi, ambayo ni chakula kikuu kwa familia nyingi za wafugaji, yamekuwa ghali zaidi, hali inayoongeza mzigo wa maisha.
Kwa mujibu wa wakazi wa Terrat, bei ya mahindi kwa sasa imepanda kwa zaidi ya asilimia 50 katika miezi michache iliyopita. Wakati huo huo, mifugo ambayo ndiyo kitega uchumi kikuu kwa jamii ya wafugaji, inapoteza thamani sokoni kutokana na athari za ukame, hali inayosababisha mifugo kuwa dhaifu na kushindwa kupata soko la uhakika.
Takwimu kutoka soko la Terrat zinaonyesha kuwa kwa sasa, bei ya debe moja la mahindi imepanda kutoka TZS 25,000 hadi kufikia TZS 40,000, ongezeko ambalo ni changamoto kubwa kwa familia zinazotegemea mifugo kama chanzo kikuu cha kipato. Wafugaji wengi wanapambana kupata fedha za kununua chakula huku mifugo yao ikiendelea kupoteza thamani.