
Vijana wanachukua asilimia 46 ya watu wote nchini Tanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kwa tafsiri, kijana ni mtu mwenye umri wa miaka 15 hadi 35. Licha ya kuwa kundi kubwa katika jamii, bado wanakumbana na changamoto nyingi katika kushiriki kwenye siasa na nafasi za maamuzi.
Licha ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007) kusisitiza ushiriki wao katika maamuzi, vijana wengi wanasema kuwa hali ngumu ya kiuchumi inawafanya washindwe kushiriki kwenye chaguzi kwa sababu ya gharama kubwa za kugombea nafasi za uongozi.
Baadhi ya vijana kutoka mkoani Arusha wanasema kuwa kipato kidogo ni changamoto kubwa inayowakabili, kwani michakato ya uchaguzi inahitaji rasilimali za kifedha ambazo wengi wao hawana. Wanadai kuwa gharama za kugombea nafasi za uongozi ni kubwa na hivyo kuwafanya washindwe kushiriki kikamilifu kwenye siasa.
[Sauti ya baadhi ya vijana kutoka mkoani Arusha]
Wazee katika kata ya Ngarenaro mkoani Arusha wanaeleza kuwa, licha ya vijana kuwa na nguvu, ubunifu na maono mapya, bado kuna mtazamo katika jamii kuwa uongozi unapaswa kushikwa na watu wenye umri mkubwa zaidi. Wanaeleza kuwa kijana anaweza kuwa na uwezo wa kuongoza, lakini bado jamii haijaweka imani kubwa kwao kushika nafasi za juu za maamuzi.
[Sauti ya baadhi ya wazee wa mtaa wa Mita 200, kata ya Ngarenaro, Arusha]
Ili kuhakikisha kuwa vijana wanapata nafasi ya kushiriki kwenye maamuzi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mita Mia Mbili, Peter Lukumay, anasema kuwa kuna juhudi za kuwaandaa vijana kushika nafasi za uongozi kwa kuwashirikisha katika masuala ya kijamii na kuwapa elimu ya uongozi. Anasema kuwa ni muhimu kuwa na mkakati wa kuwahamasisha vijana, kuwaelimisha kuhusu siasa na kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali.
[Sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mita Mia Mbili, kata ya Ngarenaro]
Vijana kutoka Arusha wanasema kuwa ili waweze kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo, wanahitaji kupewa fursa za kiuchumi ili waweze kugharamia michakato ya uchaguzi, kupewa elimu ya uongozi na kushirikishwa katika maamuzi kuanzia ngazi za mtaa hadi taifa. Wanasema kuwa jamii inapaswa kubadili mtazamo wake na kuamini kuwa vijana wanaweza kuwa viongozi bora wa kesho, ikiwa watawezeshwa na kupewa nafasi sawa na makundi mengine katika jamii.
[Sauti ya baadhi ya vijana na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mita Mia Mbili, mkoani Arusha]