
Na nyangusi Ole Sang’ida
Wafanyabiashara wadogo maarufu kama Mama Lishe na Baba Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wamepokea kwa furaha majiko ya gesi yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuboresha shughuli zao za upishi pamoja na kuhifadhi mazingira.
Katika zoezi la kugawa majiko hayo lililofanyika jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Bw. Seleman Msumi amesema majiko hayo 50 ni utekelezaji wa ajenda ya Rais Samia katika kuhakikisha Watanzania wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Ojungu Salekwa amesema zoezi hilo ni awamu ya kwanza, likiwa na lengo la kuhifadhi mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni.
Akizungumza kwa niaba ya Mama Lishe, Neema Burra kutoka Kata ya Oljoro amesema wamekuwa wakipata changamoto kubwa ikiwemo kuumwa macho kutokana na moshi wa kuni na kwamba matumizi ya gesi yataokoa muda na kuwawezesha kufanya biashara kwa ufanisi zaidi.
“Namshukuru sana Rais Samia kwa kutupatia gesi, imeniondolea madhara ya kiafya kama maumivu ya macho yanayosababishwa na moshi wa kuni. Gesi ni safi kwa afya, mazingira na biashara yetu,” amesema Neema.
Zoezi hili limetajwa kuwa litasaidia kupunguza ukataji miti, kulinda mazingira na kuinua uchumi wa wafanyabiashara wadogo katika halmashauri hiyo.

Kwa habari zaidi tembelea tovuti yetu: www.ors-radio.co.tz