
Na Nyangusi Ole Sang’ida
Kongamano la Kanda ya Kaskazini kuelekea Siku ya Wanawake Duniani 2025 limefanyika mkoani Arusha, likihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (MB), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ushiriki wa Wanawake katika Utalii na Maliasili; Miaka 30 ya Azimio la Beijing.”
Dkt. Stergomena amepongeza hatua kubwa zilizofikiwa na Tanzania katika miaka mitatu tangu Azimio la Beijing, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutambua nafasi ya mwanamke katika jamii. Aidha, ameeleza kuwa juhudi za kuinua wanawake zimezaa matunda kwenye uongozi, uchumi, elimu, afya, na haki za binadamu.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Mwanaid Mwanahamis, amesema wizara imeratibu kongamano hili ili kuhakikisha kila mshiriki anapata fursa sawa, na kwamba wanawake sasa wanatambua nguvu zao – ndiyo maana wanaongoza katika nyanja mbalimbali.

Naye Jakiline Mafuru, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wenye Makampuni ya Utalii Tanzania, ameonesha furaha yake kwa ukuaji wa sekta ya utalii ambayo imewajumuisha wanawake madereva, wapokezi, na hata waongozaji watalii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa. Wajasiriamali walioshiriki kongamano hili wamesisitiza kuwa fursa hizo zinawafikia moja kwa moja, zikiwapa hamasa zaidi ya kupiga hatua mbele