
Baraza la madiwani jiji la Arusha limefungwa rasmi katika hafla ya kipekee iliyoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh. Mohamed Mchechengerwa. Katika hotuba yake, Waziri Mchechengerwa aliwapongeza madiwani kwa kazi yao ya juhudi kubwa na aliwahakikishia kuwa vifaa walivyotumia, kama vishikwambi, vitakuwa mali yao rasmi.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, aliwataka madiwani kuhakikisha usalama na ulinzi katika maeneo yao, na kuendeleza miradi ya maendeleo ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, aliwahimiza wananchi wote kuhudhuria huduma za afya za bure kuanzia Juni 23 hadi 29, ambapo kutapatikana dawa na vipimo vyote bure. Alisisitiza umuhimu wa kulinda amani wakati wa uchaguzi ili kulinda uchumi na sekta ya utalii ya jiji.
Diwani wa kata ya Ngarenaro, Isaya Doita, aliwashukuru madiwani wenzake na kuhimiza umoja na amani katika mchakato wa uchaguzi. Aliweka bayana kuwa:
“Tumefanya kazi kubwa katika miaka mitano iliyopita, na sasa tunaanza likizo ya miezi minne tukihimiza amani, umoja, na viongozi bora watakaojenga taifa kwa utulivu.”
Waziri Mchechengerwa aliongeza kuwa mafanikio ya Awamu ya Sita yamefikiwa kwa usimamizi wa mabaraza ya madiwani nchi nzima, na wengi wanatarajiwa kurudi kwenye awamu ya pili. Alisema vifaa vilivyotumiwa awali vitakuwa mali yao hadi watakapokwenda.
Baraza la madiwani jiji la Arusha limepongezwa kwa ushirikiano mzuri na mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, jambo linaloleta matumaini ya maendeleo endelevu kwa jiji zima.
