
World Sickle Cell Awareness Day ni siku inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 19 Juni ili kuhamasisha elimu juu ya ugonjwa wa sikoseli. Ugonjwa huu wa damu, unaosababisha mabadiliko ya seli nyekundu za damu, unaathiri mamilioni ya watu duniani, hasa katika maeneo kama Tanzania.
Katika siku hii, jumuiya za afya, serikali na wadau hufanya kampeni za kuelimisha watu kuhusu ugonjwa huu, kuondoa ubaguzi, na kuongeza msaada kwa wagonjwa na familia zao.
Dkt. Fidelis Sunday wa Hospitali ya Mkoa wa Manyara anafafanua kuwa sikoseli ni ugonjwa unaosababisha seli za damu kuwa za umbo la sikio, kuziba mishipa ya damu na kusababisha maumivu makali, maambukizi na matatizo makubwa kiafya.
“Matibabu tunazotoa ni kuzuia maumivu, kuzuia damu kuganda na kuzuia maambukizi. Kuchelewa kupata matibabu kunaweza kusababisha matatizo makubwa kama kiharusi na hata kifo,” anasema Dkt. Fidelis.
Dkt. Fidelis anasisitiza umuhimu wa vipimo vya mapema:
“Wanandoa wanapaswa kufanya vipimo vya vinasaba kabla ya kuanza maisha ya ndoa ili kupunguza hatari kwa watoto wao.”
Kwa kuadhimisha siku hii, tunahimiza jamii kufahamu zaidi, kuhudhuria vituo vya afya, na kuhakikisha matibabu ya sikoseli yanapatikana kwa wote ili kuboresha maisha ya wagonjwa.