
Katika jitihada za kuboresha afya ya mifugo, hususan mbuzi na kondoo, wataalamu wa mifugo kutoka Wilaya ya Simanjiro wamekutana leo katika ukumbi wa mikutano wa Ilaramata (Manyara Hall) kujadili mradi mpya wa afya ya mifugo. Mradi huu unafadhiliwa na Chuo Kikuu cha Glasgow, Uingereza, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), na unalenga kutumia app ya simu kusaidia watoa huduma ngazi ya jamii.
Dkt. Yassin Mshana, mtaalamu wa mifugo kutoka idara ya Mifugo, Kilimo, na Uvuvi Wilaya ya Simanjiro, amesema kuwa “app hii itawezesha wahudumu wa afya ya mifugo kutambua magonjwa kwa urahisi na kupata mwongozo wa tiba sahihi.” App hiyo itakuwa suluhisho kwa changamoto ya kutofahamu magonjwa yanayoathiri wanyama wadogo na pia kusaidia mawasiliano kati ya watoa huduma na wataalamu wa mifugo.
Mmoja wa wataalamu wa mifugo, Tila Shinini, ameongeza kuwa mara nyingi wahudumu wa jamii wanakabiliwa na changamoto ya kutambua magonjwa sahihi kutokana na dalili zinazofanana, lakini kupitia app hii, “wahudumu wataweza kuingiza dalili walizoziona kwa mifugo, na mfumo wa app utawasaidia kupata majibu sahihi na ushauri wa tiba.“
Changamoto nyingine kubwa iliyobainishwa na wahudumu wa mifugo ni ukosefu wa mtandao wa mawasiliano na usafiri wa kuwafikia wafugaji kwa wakati. Mara nyingi, wahudumu wanakosa mafuta ya pikipiki au kushindwa kuwasiliana na wataalamu wa mifugo. “App hii itasaidia kupunguza changamoto hizi kwa kuwezesha utambuzi wa magonjwa hata bila mawasiliano ya moja kwa moja na daktari wa mifugo.”
Wadau wa mifugo wamepongeza mradi huu na kupendekeza kuwa ili kufanikisha utekelezaji wake kwa ufanisi zaidi, app itafsiriwe kwa Kiswahili ili iwe rahisi kutumiwa na wahudumu wa jamii. Pia, wameomba kuwepo na mafunzo maalum kwa watoa huduma ili kuhakikisha wanaelewa matumizi ya app hii kikamilifu.
Mradi huu unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya ya mifugo Simanjiro na kusaidia wafugaji kupata huduma bora kwa wanyama wao, kupunguza vifo vya mifugo, na kuongeza uzalishaji wa mifugo kwa jamii ya wafugaji.