![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2024/12/ukeketaji.jpg)
Jifunze simulizi ya Recho Thomas, binti wa jamii ya Wamasai aliyeepuka ukeketaji na sasa ni sauti ya mabadiliko. Soma na Sikiliza jinsi alivyoshinda mila potofu na juhudi za kumaliza ukatili huu.
Katika kipindi hiki cha likizo ya Desemba, jamii nyingi za kifugaji hufanya sherehe kubwa, ikiwemo ukeketaji wa mabinti kama sehemu ya mila na tamaduni za zamani. Lakini simulizi ya Recho Thomas ni ya kipekee. Akiwa binti wa jamii ya Wamasai, Recho alikataa kufuata mila hii na sasa anapaza sauti kwa niaba ya wasichana wengine walio hatarini.
Changamoto Anazopitia Wasichana Wasio Keketwa
Kwa mujibu wa ripoti ya Demographic and Health Survey ya 2015-2016, asilimia 58 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 katika Mkoa wa Manyara wamefanyiwa ukeketaji, hali inayoonyesha ukubwa wa tatizo. Lakini kwa wale waliokataa mila hii, maisha si rahisi. Recho anasema:
“Mara nyingi unakutana na unyanyapaa kutoka kwa jamii, familia, na hata marafiki. Lakini nilijua uamuzi wangu ulikuwa sahihi.”
Kwa msaada wa mashirika kama Pastoral Women Council (PWC),na Taasisi za Dini Recho alipata ujasiri wa kusimama imara dhidi ya shinikizo la jamii. Sasa, anahamasisha wasichana wengine kupinga ukatili huu kupitia majukwaa ya kijamii na semina za uhamasishaji.
Nini Kimefanyika Kupinga Ukeketaji?
Afisa Uga wa PWC, Grace Mbario Tayayi, anasema:
“Elimu ni silaha kubwa. Tunawahamasisha wazazi na viongozi wa kijamii kubadilisha mitazamo yao kuhusu mila hizi. Hali inabadilika, ingawa bado kuna changamoto.”