Viongozi wa Tarafa ya Terrat Wataka Wanafunzi Wafike Shuleni Ifikapo Januari 25

Ni wiki moja tangu shule za msingi na sekondari kufunguliwa rasmi nchini Tanzania, huku wazazi na viongozi wakionyesha jitihada zao kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati. Hata hivyo, hali si shwari katika Tarafa ya Terrat, Wilaya ya Simanjiro, Manyara, ambapo idadi ndogo ya wanafunzi wa awali, darasa la kwanza, na kidato cha kwanza imeonekana kuripoti shuleni.

Kufuatia hali hiyo, Katibu Tarafa wa Terrat, Bw. Lekishoni Kiruswa, ametoa maagizo kwa wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji, walimu wakuu, watendaji wa vijiji, pamoja na waratibu wa elimu kata kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanafika shuleni ifikapo Januari 25, 2025.

“Kila mwenyekiti wa kitongoji chako shirikiana na mtendaji shirikiana na mwalimu mkuu watoto wote waripoti” alisema Bw. Lekishoni Kiruswa.

Changamoto za Utoro na Ufaulu Mdogo

Bw. Lekishoni alibainisha kuwa utoro ni changamoto kubwa katika tarafa hiyo, tatizo linalochangiwa na baadhi ya wazazi kushirikiana na wanafunzi, hali inayosababisha matokeo mabaya katika mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili kwa mwaka wa masomo wa 2024.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Katibu Tarafa huyo amewataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana kutokomeza utoro na kuwachukulia hatua wale wote wanaochangia hali hiyo.

“Tuna utoro rejareja na ule utoro wenyewe ndugu viongozi tukapambane na utoro,walimu nafikiri taarifa mnazitoa,kama mnaona mtendaji analegalega mpe mwenyekiti” alisisitiza Bw. Lekishon

Kukabiliana na Changamoto ya Mimba Mashuleni

Tatizo la mimba mashuleni pia limebainishwa kuwa changamoto kubwa katika Tarafa ya Terrat, hasa kwa wasichana wa shule za msingi na sekondari. Bw. Lekishoni ametoa wito kwa viongozi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa karibu ili kupambana na tatizo hilo linaloathiri mustakabali wa wanafunzi na maendeleo ya jamii.

“Ndugu zangu kuna mimba mashuleni si kweli? na mimba zingine zinamalizwa juu kwa juu hiyo ni hatari” alisema Bw. Lekishoni.

Jeshi la Polisi Lafafanua Mikakati

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Tarafa ya Terrat amewahimiza viongozi hao kushirikiana na askari kata waliopo katika kila kata ili kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shule kwa wakati. Aidha, Kamanda huyo amesisitiza kuwa endapo kutatokea tukio la mwanafunzi kukatishwa masomo kwa sababu ya ujauzito, taarifa zitolewe mara moja kwa Jeshi la Polisi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“Kila kata inaaskari wake tena ni Inspekta shirikianeni na wale askari kule,” alisema Kamanda wa Polisi.

Hatua za Haraka

Bw. Lekishoni ameweka wazi kuwa utekelezaji wa maagizo haya utafuatiliwa kwa karibu, na matarajio ni kuona kila mwanafunzi anaanza masomo ifikapo Januari 25.

Hii ni sehemu ya juhudi za viongozi wa Tarafa ya Terrat kuhakikisha elimu inabaki kuwa kipaumbele cha juu, na changamoto kama utoro na mimba mashuleni zinatatuliwa kwa kushirikiana na jamii nzima.

Andika maoni yako kuhusu jitihada hizi za serikali ya tarafa ya Terrat katika kurasa zetu za mitandao ya kijamii @orkonereifmradio.

Related Posts

Polisi Arusha Waimarisha Ukaguzi wa Mabasi Kukabiliana na Ajali

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanya ukaguzi maalumu wa mabasi ya abiria ili kudhibiti ajali kutokana na ongezeko la wasafiri kipindi cha likizo za shule. Madereva wamehimizwa kuzingatia sheria…

Continue reading
Madereva 800 Wapatiwa Mafunzo Maalumu Kuelekea Msimu wa Utalii Arusha

Zaidi ya madereva 800 wa magari ya utalii mkoani Arusha wamepatiwa mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ikiwa ni maandalizi ya msimu wa utalii (high…

Continue reading

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You Missed

Polisi Arusha Waimarisha Ukaguzi wa Mabasi Kukabiliana na Ajali

Polisi Arusha Waimarisha Ukaguzi wa Mabasi Kukabiliana na Ajali

Madereva 800 Wapatiwa Mafunzo Maalumu Kuelekea Msimu wa Utalii Arusha

Madereva 800 Wapatiwa Mafunzo Maalumu Kuelekea Msimu wa Utalii Arusha

Kijana auawa kwa kisu Arusha, wananchi wachoma nyumba ya mtuhumiwa

Kijana auawa kwa kisu Arusha, wananchi wachoma nyumba ya mtuhumiwa

Jamii ya Maa Iwe Makini na Wanaotaka Kuigombanisha na Serikali – Fred Lowassa

Jamii ya Maa Iwe Makini na Wanaotaka Kuigombanisha na Serikali – Fred Lowassa

Madereva wa Serikali Arusha Wawezeshwa kwa Mafunzo ya Usalama Barabarani

Madereva wa Serikali Arusha Wawezeshwa kwa Mafunzo ya Usalama Barabarani

Wadau Waungana Kunusuru Mazingira ya Maasai Steppe

Wadau Waungana Kunusuru Mazingira ya Maasai Steppe
Enable Notifications OK No thanks