![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/B-1.jpg)
UN Women kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli wamefanya mdahalo mkubwa Januari 8, 2025, katika Kata ya Naalarami, wenye lengo la kuimarisha nafasi ya mwanamke kiuchumi, kisiasa, na kiuongozi. Tukio hili limewaleta pamoja viongozi wa mila (malaigwanani), viongozi wa dini, na wanajamii ili kujadili masuala ya kijinsia, haki za wanawake, na maendeleo ya jamii.
Hamasa kwa Wanawake
Bi. Aimosaria Minja, mratibu wa UN Women, amewahamasisha wanawake kujiunga na vikundi vya vikoba ili kuimarisha hali zao za kiuchumi. “Shughuli za maendeleo kama hizi zinatoa nafasi kwa wanawake kuwekeza kwa ajili ya familia zao na jamii nzima,” amesema.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/C.jpg)
Miriam Ndakaji, mkazi wa kijiji cha Engorika, amepongeza juhudi za UN Women na kuongeza kuwa wanawake sasa wameamka na kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi, hasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Hali ya wanawake sasa haiwezi kulinganishwa na zamani. Tumeelimishwa na tumepata ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema.
Maoni ya Malaigwanani na Viongozi wa Jamii
Laigwanani Pelo Saning’o kutoka kijiji cha Lengloriti amepongeza midahalo ya UN Women kwa kubadili mtazamo wa jamii kuhusu wanawake. “Leo hii wanawake wanashika nafasi muhimu za uongozi, tofauti na zamani,” amesema.
Mwalimu Emmanuel Zagila wa shule ya msingi Lengloriti ameongeza kuwa maendeleo ya wanawake pia yanaonekana katika elimu. Watoto wa kike wameanza kuongoza darasani, tofauti na zamani ambapo walinyimwa fursa ya kusoma.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/A.jpg)
Tathmini ya Matokeo
Bi. Aimosaria Minja amehitimisha mdahalo huo kwa kupongeza wanawake wa Kata ya Naalarami kwa mafanikio yao makubwa, hasa katika kujitokeza kugombea nafasi za uongozi. “Tumeona maendeleo makubwa sana, na juhudi hizi ni mwanga wa maisha bora kwa wanawake na jamii kwa ujumla,” amesema.
Mdahalo huu unaakisi juhudi za UN Women katika kuleta mabadiliko chanya kwa wanawake, hasa mwaka huu wa 2025 ambapo Tanzania inajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.
#MaendeleoKwaWanawake #Uchaguzi2025 #ORSRadio