
Katika kijiji cha Engonongoi, wilayani Simanjiro, kuna familia ambayo imeamua kupita njia isiyozoeleka na ambayo sasa imekuwa mfano wa kuigwa na jamii yao. Ni familia ya Thomas Lazaro na mkewe Naitapoaki Thomas, ambao wameamua kushirikiana kwa karibu katika kila uamuzi wa kifamilia iwe ni kuhusu mifugo, kilimo, biashara au maendeleo ya nyumbani.
Katika jamii nyingi za kifugaji, wanaume hutazamwa kama watoa uamuzi wa mwisho, huku wanawake wakibaki nyuma ya pazia. Lakini kwa Thomas, mtazamo huu wa zamani haufai tena. Akiwa amekulia kwenye jamii yenye mila zinazotenganisha majukumu ya jinsia, Thomas ameona nguvu iliyopo kwenye ushirikiano na mkewe katika maamuzi ya kila siku.
“Tunapokaa chini na kupanga kwa pamoja, tunajua nini tunalenga. Hakuna ugomvi, Ushirikiano wetu umezaa matunda,” anasema Thomas akiwa na tabasamu na ameketi juu ya pikipiki yake.
Mwaka jana, Thomas na Naitapoaki walikubaliana jambo moja muhimu: kutokuuzia mtu mwingine wala kukodisha shamba lao. Badala yake, walilima wenyewe, wakachapa kazi kwa bidii na kufanikisha mavuno ya kutosha. Kilichofuata ni uamuzi wa pamoja wa kuuza mazao yao sokoni na kuwekeza faida hiyo kwenye biashara ndogo.
Licha ya mafanikio haya, si kila mtu kijijini anapokea mabadiliko haya kwa urahisi. Naitapoaki anasema baadhi ya majirani wameshindwa kuamini kuwa mumewe anamshirikisha katika maamuzi ya familia.
“Wengine wanasema labda nina dawa” anasisitiza.
Kwa upande wa Thomas, anasema haoni haja ya kuwa kiongozi wa familia peke yake. Kwake, kuvunjilia mbali mila zinazomnyima mwanamke nafasi ya kutoa sauti ni hatua ya mabadiliko ya kweli.
“Hakuna dawa. Kinachohitajika ni kuelewa kuwa familia siyo mtu mmoja,” anasema kwa msisitizo.
Ushirikiano huu umechangia sio tu kuongeza kipato chao, bali pia umekuwa darasa kwa wengine waliokuwa na mitazamo tofauti. Thomas na Naitapoaki sasa ni kielelezo cha jinsi usawa wa kijinsia katika maamuzi ya kifamilia unavyoweza kujenga msingi imara wa maendeleo.
Katika makala fupi ya sauti, familia hii imeeleza kwa sauti zao wenyewe jinsi walivyopitia changamoto, walivyoshirikiana kwa upendo, na hatimaye kufanikisha ndoto yao ya kuwa na uhuru wa kiuchumi na utulivu wa kifamilia.
🎧 Sikiliza hapa makala hii kamili ya familia ya Thomas Lazaro na Naitapoaki wakieleza safari yao ya matumaini, maamuzi na mabadiliko kutoka kijiji cha Engonongoi.