![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/1-1-scaled.jpg)
Mgogoro wa umiliki wa ardhi katika mpaka wa Kijiji cha Terrat, Kata ya Terrat, na Kijiji cha Sukuro, Kata ya Komolo, umeibua mjadala mkubwa katika mkutano mkuu wa kijiji cha Terrat uliofanyika Januari 13, 2024. Eneo lenye mgogoro linadaiwa kumilikiwa na mkazi wa Terrat, Bwana Marko Sangeti, huku serikali ya kijiji hicho ikisisitiza kuwa ni mali ya kijiji,Eneo likiwa ni zaidi ya hekari 200.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/IMG_20250113_135116_987-1024x768.jpg)
Katika mkutano huo, Bwana Marko Sangeti alisisitiza kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo na akaeleza kuwa serikali ya kijiji inataka kumnyang’anya ardhi yake kwa madai kuwa ni mali ya kijiji.
“Ninamiliki eneo hili kihalali, na nina nyaraka zote zinazothibitisha. Tatizo ni kwamba mgogoro huu unachukuliwa kisiasa zaidi kila uchaguzi unapokaribia,” alisema Sangeti.
Historia ya Mgogoro
Aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji cha Terrat miaka ya 1980, Bwana Isaya Nelukendo, alisema kuwa eneo hilo ni mali ya kijiji na si ya mtu binafsi.
“Tulipoweka mkataba tuliweka mkataba wa kijiji cha terrat wala siyo mtu mmoja,” alisema Nelukendo.
Isack Abraham, aliyekuwa mwakilishi wa kijiji cha Terrat wakati wa makabidhiano ya mkataba na taasisi inayomiliki ranchi ya Ormoti, aliunga mkono madai ya Bwana Sangeti. Aidha, Laigwanani Jacob Nduya, alifafanua mkataba huo, akisema kuwa ulikuwa na vipengele vinavyobainisha umiliki wa eneo hilo.
Mzozo Unavyoendelea
Mwenyekiti wa sasa wa kijiji cha Terrat, Ndg. Kone Medukenya, alisema kuwa mgogoro huo umekuwa ukijirudia mara kwa mara na unahitaji suluhisho la kudumu.
“Tulisema tuletee nyaraka ili tumalize huu mgogoro” alisema Medukenya.
Njia ya Suluhisho
Diwani wa Kata ya Terrat, Ndg. Jackson Matery, aliishauri serikali ya kijiji kuunda kamati ndogo ya kuchunguza umiliki wa eneo hilo na kutoa mapendekezo ya suluhisho.
“Naomba niombe kitu kimoja hatuwezi kumuambia Marko alete Documents hapa tuzisome mbele ya hadhara,” alisema Matery.
Mgogoro wa Kisiasa?
Bwana Sangeti aliongeza kuwa mgogoro huo unachochewa zaidi na siasa, hasa wakati wa uchaguzi.
“Kila wakati uchaguzi unapokaribia, ardhi yangu inageuka sehemu ya kampeni za kisiasa.” alisisitiza.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/IMG_20250113_135923_968-1024x768.jpg)
Mgogoro huu wa ardhi unaonyesha changamoto kubwa zinazokabili usimamizi wa rasilimali ardhi nchini Tanzania, hasa katika maeneo ya vijijini ambako mipaka ya ardhi haijabainishwa wazi.