
Katika kijiji cha Loswaki, wilayani Simanjiro, Marta Noah ameandika historia ndogo lakini yenye ujumbe mkubwa. Katika jamii ya Kimasai ambako mila na desturi zimekuwa kizuizi kwa wanawake kumiliki ardhi, Martha ni miongoni mwa wachache waliothubutu na kufanikisha ndoto hiyo kupitia maelewano na mume wake.
Kupitia kipindi cha Nijuze cha Orkonerei FM Radio, Marta ameeleza jinsi alivyomwomba mume wake amtambue kwa kumpatia sehemu ya ardhi rasmi. Tangu mwaka 2019, baada ya kupata mtoto wao wa tatu, alikabidhiwa heka mbili ambazo amekuwa akizitumia kwa kilimo, ufugaji wa mbuzi na kuinua hali ya maisha ya familia.
“Nikaona nami nastahili kuwa na maendeleo yangu mwenyewe,” anasema Marta, ambaye sasa anamiliki mali binafsi ikiwemo mbuzi, meza, viti, na samani nyingine.
Mume wake anasema awali haikuwa rahisi, kutokana na mila, lakini aliona faida za usawa na maelewano ndani ya familia. “Maneno yapo,” anasema, “lakini niliona mazingira yetu. Sasa sina presha, yeye anajitegemea, hata watoto anawasaidia.”
Hadithi ya Marta ni mfano wa wazi wa mabadiliko yanayowezekana katika jamii za kifugaji kupitia elimu, upendo na ushirikiano wa familia.