
Na Nyangusi ole Sang’ida
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, ametoa tathmini yakinifu kuhusu maendeleo ya zoezi la kusikilizwa kwa wananchi mkoani. Tangu kuanza kwa huduma hii, iliyolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, idadi ya watu waliosikilizwa imefikia 1,844 hadi tarehe 7 Machi 2025.
Katika mchakato huo, migogoro 677 iliwasilishwa na kusajiliwa. Kati ya hiyo, migogoro 136 tayari imepatiwa ufumbuzi kwa njia ya maridhiano na makubaliano kati ya pande husika. Hatua hii imepongezwa kwa nguvu kubwa, ikionesha jinsi msaada wa kisheria unavyoweza kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kusaidia wananchi kupata suluhisho kwa haraka.
Aidha, wale wenye kesi zinazohusu ndoa, mirathi, na masuala ya madai wameelekezwa njia sahihi za kimahakama ili kuhakikishiwa haki zao. Msambazi anasisitiza kuwa jukumu la Wizara ni kuhakikisha wananchi wanapata mwongozo stahiki, hasa pale wanapokosa uelewa wa sheria au kushindwa kumudu gharama za uwakilishi.
Kwa upande mwingine, wananchi wenyewe wametoa ushuhuda kuhusu tija ya huduma hii. Mama Samia Abrahamu Miagie, mmoja wa waliotumia huduma ya msaada wa kisheria, amepongeza sana juhudi za timu hiyo, akieleza kwamba wao ‘kuingilia kati’ ndiko kulikowezesha maelewano kufikiwa. Vilevile, Adela Robert Molel, mkazi wa Sakina, ameainisha shukrani zake baada ya kesi ya mirathi kuwekewa msingi wa haki, akitoa wito kwa wananchi wengine kujitokeza bila woga pale wanapohitaji msaada.