Mtaalamu wa sheria, Ndg. Saitabau Laadapi, mwanafunzi wa shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira jijini Arusha, ametoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mgogoro wa ardhi unaomhusisha Bwana Marko Sangeti na Kijiji cha Terrat, wilayani Simanjiro. Akizungumza na Orkonerei FM Radio kwa njia ya simu, Laadapi ameeleza kwa kina masuala ya kisheria yanayohusiana na umiliki wa ardhi ya kijiji na changamoto zinazochangia migogoro kama huu.
Kwa mujibu wa sheria za ardhi nchini, hasa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ardhi ya kijiji inapaswa kuwa chini ya umiliki wa wananchi wa kijiji kupitia serikali yao ya kijiji. Hata hivyo, mtu binafsi anaweza kumiliki ardhi ya kijiji endapo taratibu za kisheria zitafuatwa, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa idhini ya mkutano mkuu wa kijiji na nyaraka rasmi kama hati miliki au barua ya umiliki kutoka serikali ya kijiji.
Akizungumzia mgogoro wa sasa, Ndg. Laadapi amesema kuwa, iwapo Bwana Marko Sangeti ana nyaraka zote halali zinazothibitisha umiliki wa ardhi hiyo, basi kisheria ardhi hiyo ni mali yake. Hata hivyo, kama nyaraka hazijakamilika au hazipo, ardhi hiyo inapaswa kurudi kwa umiliki wa kijiji kwa mujibu wa sheria.
“Muhimu ni kuhakikisha kuwa nyaraka zote muhimu zipo ili kuthibitisha umiliki halali wa ardhi. Kwa kawaida, nyaraka kama hati miliki, barua za idhini kutoka kijiji, na maazimio ya mkutano mkuu wa kijiji ndio anachotakiwa kuwa nacho Mzee Marko Sangeti,” alisema Laadapi.
Aidha, mtaalamu huyo ameeleza kuwa sheria huangalia mambo mbalimbali katika kutatua migogoro ya ardhi, ikiwa ni pamoja na ushahidi wa nyaraka, maamuzi ya mkutano mkuu wa kijiji, na hatua zilizochukuliwa na serikali ya kijiji katika kugawa ardhi. Amesisitiza kuwa serikali ya kijiji ina jukumu la kuhakikisha kuwa ardhi inagawiwa kwa uwazi,sawa kwa kila mwanakijiji na kwa kufuata taratibu za kisheria ili kuepusha migogoro.
Ndg. Laadapi ameonya kuwa migogoro mingi ya ardhi vijijini hutokana na ukiukwaji wa sheria na mara nyingine rushwa katika mchakato wa kugawa ardhi. Amesema kuwa ni jukumu la viongozi wa kijiji kufuata taratibu na kuwashirikisha wananchi ipasavyo ili kuhakikisha haki inatendeka.
Pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu mgogoro huo, Laadapi pia ametoa mapendekezo ya hatua za kushughulikia migogoro ya ardhi kwa njia za kisheria. Ameeleza kuwa, kwa kawaida, migogoro ya aina hii inapaswa kijiji kutatu na ikishindikana hupelekwa Mahakamani, ambako pande zote zinapata nafasi ya kuwasilisha nyaraka na ushahidi wao.
“Endapo itathibitishwa kuwa ardhi ni mali ya Bwana Sangeti, basi serikali ya kijiji haina cha kufanya. Vinginevyo, ikiwa nyaraka hazipo, basi ardhi hiyo inapaswa kurudi kwenye umiliki wa kijiji” aliongeza.
Ndg. Laadapi pia ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanahusika katika michakato yote ya ugawaji na umilikishwaji wa ardhi na maamuzi yoyote yanayofanywa juu ya ardhi ya vijiji wanahusika. Aidha, amewashauri viongozi wa vijiji kuhakikisha wanazingatia sheria na kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao za kisheria ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara
Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii nyingi za vijijini, huku kukosekana kwa uwazi na uelewa wa sheria za ardhi kikiwa chanzo kikuu cha mivutano. Ndg. Laadapi ameonya kuwa, iwapo migogoro ya aina hii haitashughulikiwa ipasavyo, inaweza kusababisha athari kubwa kwa maendeleo ya kijamii kwani ukubwa wa mgogoro utaongezeka na utafikia pabaya.
Sikiliza mahojiano hayo kwa njia ya simu hapa chini.
Makala mazuri 👏👏