

“Serikali yetu haiwezi kufurahia kuona jamii yetu inahangaika na masuala ya malisho. Nimejiridhisha kwamba maeneo yetu yataendelea kutumika kwa malisho na mafunzo ya kijeshi,” alisema Lowassa.
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Fredrick Lowassa amewataka wananchi wa jamii ya Maa kuwa na umoja na uangalifu dhidi ya watu wanaotaka kuwagombanisha na serikali kwa malengo yao binafsi.
Akizungumza kwenye sherehe ya vijana maarufu kama “Engipaata oo Irmegoliki” iliyofanyika Kata ya Meserani Mei 25, 2025, Mhe. Lowassa amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu aliowaita “madalali” kuitumia jamii hiyo kuleta migogoro ili wao wapate manufaa.
Amesema serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni serikali sikivu na yenye nia njema kwa jamii ya Maa, hasa katika kulinda maeneo yao ya malisho.
“Serikali yetu haiwezi kufurahia kuona jamii yetu inahangaika na masuala ya malisho. Nimemtafuta Waziri wa Ulinzi na nimejiridhisha kwamba maeneo yetu yataendelea kutumika kwa malisho na mafunzo ya kijeshi,” alisema Lowassa.
Aidha, Lowassa amewataka wananchi hao kuhakikisha wanaendelea kuiunga mkono serikali ya Chama cha Mapinduzi ili kulinda maslahi yao na kuhakikisha maendeleo endelevu yanafikiwa katika jamii ya Maa.
Amewataka wananchi kuwa watulivu, wenye umoja na kuendelea kushirikiana na serikali katika kusimamia masuala yao muhimu bila kudanganywa na watu wenye nia ovu.