
Katika jamii nyingi za Kitanzania, ujauzito ni safari ambayo inapaswa kuwa ya wawili, lakini kwa wanawake wengi wa maeneo ya vijijini kama Terrat, safari hiyo inageuka kuwa ya upweke, huzuni na changamoto kubwa.
Kupitia simulizi ya sauti yenye mguso wa kipekee, inayojulikana kama “Mwambie Nimesafiri,” mtangazaji na mwandishi wa Orkonerei FM Radio, Isack Dickson, anachora picha halisi ya namna mila na desturi zimewafanya baadhi ya wanaume kushindwa kushiriki kikamilifu katika huduma za afya ya uzazi kwa wake zao.
🎧 Sikiliza Simulizi Kamili Hapa:
👉 [Bonyeza kusikiliza]
Katika sauti hiyo, tunasikia ushuhuda kutoka kwa Magdalena Soipe, mkazi wa Terrat, ambaye anaeleza kwa uchungu jinsi ambavyo wanawake wanahangaika kupata huduma za kliniki bila msaada wa waume zao. Anasema baadhi ya wanaume huona ni aibu kufuatana na wake zao kliniki, wengine wakitumia visingizio vya “kusafiri.”
“Unaumwa, umechoka, lakini mume wako hayupo. Wanaume wanadhani ni kazi ya mwanamke tu. Lakini siyo hivyo,” anasema Magdalena kwa sauti ya uchungu.
Kwa upande mwingine, mwanaume mmoja anaeleza changamoto ya uoga na hofu iliyojengwa na jamii kwa wanaume wanaoshiriki katika afya ya wake zao, akisema:
“Wengine wanahisi wataulizwa maswali ya ndoa zao… au daktari atagundua mambo yao ya ndani.”
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi huongeza usalama wa ujauzito na ustawi wa mtoto. Lakini katika jamii zetu, bado kuna ukimya na visingizio vinavyoacha wanawake wakiwa peke yao katika safari hiyo nyeti.
“Mila si sababu ya kumwacha mke wako apambane peke yake. Acha visingizio vya ‘nimesafiri’ – timiza wajibu wako kama mwenza na mzazi.”