UMEME WALETA MAENDELEO KATA YA TERRAT, SIMANJIRO

Nishati ya umeme imeleta mapinduzi makubwa ya maendeleo katika kata ya Terrat, mkoani Manyara. Wakazi wa eneo hili sasa wanashuhudia mabadiliko katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, elimu, afya, na ajira, tangu kuimarika kwa huduma ya umeme kupitia miradi ya usambazaji wa nishati vijijini.

Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), hadi Januari 2024, usambazaji wa umeme vijijini umefikia asilimia 80, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa. Katika kijiji cha Terrat, wafanyabiashara wanasema umeme umewaongezea tija na kuboresha mazingira ya kazi.

“Zamani tulitegemea jenereta na mishumaa, lakini sasa tunaweza kutumia vifaa vya kisasa kama friji na mashine za kuchapisha, jambo ambalo limeongeza kipato chetu,” anasema Bi. Joyce Elius, mfanyabiashara wa eneo hilo.

Katika sekta ya elimu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Terrat, Julius Maplani, anasema umeme umeleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi na walimu. “Sasa tunaweza kutumia kompyuta, projektor, na taa kwa ajili ya kujifunza hata nyakati za usiku, jambo ambalo halikuwezekana hapo awali,” anasema Maplani.

Sekta ya afya pia imenufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo Dk. Tumaini Kamkama, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Terrat, anasema vifaa vya matibabu vinavyotegemea umeme sasa vinafanya kazi bila shida. “Tunaweza kuhifadhi chanjo vizuri, kutumia mashine za uchunguzi, na hata kufanya upasuaji mdogo kwa urahisi,” anaeleza Dk. Kamkama.

Hata hivyo, licha ya mafanikio haya, bado yapo maeneo machache ambayo hayajafikiwa na umeme. Diwani wa kata ya Terrat, Ndg. Jackson Materi, anasema kuna mikakati madhubuti kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata umeme wa uhakika.

Kwa upande wa taifa, serikali kupitia Wizara ya Nishati imeweka mpango wa kufikisha umeme katika vitongoji vyote ifikapo mwaka 2025. Naibu Waziri wa Nishati, Judithi Kapinga, amethibitisha kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo.

Wakazi wa Terrat wanatarajia kuwa juhudi hizi zitaendelea ili kuhakikisha kuwa umeme unafika kila eneo na kuleta maendeleo zaidi katika jamii yao.

  • Related Posts

    Mama Anayenufaika na Kilimo cha Mboga Msimu wa Kiangazi

    Katika kipindi cha kiangazi, wakazi wa Kijiji cha Terrat hukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mboga za majani. Hata hivyo, hali hii pia inatoa fursa kwa wakulima wabunifu wanaotumia mbinu…

    Continue reading
    WAZIRI MKUU AWATAKA WAHANDISI WAZINGATIE MAADILI

    #Habari WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa awataka wahandisi wote nchini wazingatie miiko na maadili ya taalum hiyo ikiwemo kuitekeleza miradi ya ujenzi kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha halisi iliyotolewa.…

    Continue reading

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *

    You Missed

    Polisi Arusha Waimarisha Ukaguzi wa Mabasi Kukabiliana na Ajali

    Polisi Arusha Waimarisha Ukaguzi wa Mabasi Kukabiliana na Ajali

    Madereva 800 Wapatiwa Mafunzo Maalumu Kuelekea Msimu wa Utalii Arusha

    Madereva 800 Wapatiwa Mafunzo Maalumu Kuelekea Msimu wa Utalii Arusha

    Kijana auawa kwa kisu Arusha, wananchi wachoma nyumba ya mtuhumiwa

    Kijana auawa kwa kisu Arusha, wananchi wachoma nyumba ya mtuhumiwa

    Jamii ya Maa Iwe Makini na Wanaotaka Kuigombanisha na Serikali – Fred Lowassa

    Jamii ya Maa Iwe Makini na Wanaotaka Kuigombanisha na Serikali – Fred Lowassa

    Madereva wa Serikali Arusha Wawezeshwa kwa Mafunzo ya Usalama Barabarani

    Madereva wa Serikali Arusha Wawezeshwa kwa Mafunzo ya Usalama Barabarani

    Wadau Waungana Kunusuru Mazingira ya Maasai Steppe

    Wadau Waungana Kunusuru Mazingira ya Maasai Steppe
    Enable Notifications OK No thanks