![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2024/12/AKIWA-OFISINI.jpg)
Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema, amefariki dunia leo, Desemba 30, 2024, akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu. Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na Katibu wa Halmashauri ya Walei, Parokia ya Mtakatibu Martha, Salome Ntaro, ambaye ameieleza kwa masikitiko makubwa kwamba Jaji Werema alifariki mchana wa leo, huku taratibu za mazishi zikiendelea kupangwa.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2024/12/1.jpeg)
Jaji Werema alijulikana kwa ubobezi wake katika taaluma ya sheria, lakini pia aliandika historia kubwa katika sekta mbalimbali. Alianza kazi ya ualimu kama Mwalimu wa Shule ya Sekondari Shaaban Robert, jijini Dar es Salaam, mwaka 1979 hadi 1980. Baada ya hapo, alijiunga na ulingo wa sheria na kuwa wakili tangu mwaka 1984 hadi 2006. Hali hii ilimwandaa na kumfungulia njia ya uteuzi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 2009, ambapo alihudumu hadi mwaka 2014 alipojiuzulu. Pia, aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, na kutoa mchango mkubwa katika sekta ya sheria nchini.
Kwa upande mwingine, Jaji Werema alikuwa pia mwenye dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatibu Martha, ambapo alijizolea umaarufu na heshima kubwa kutokana na utendaji wake mzuri na msaada wake kwa jamii.
![](https://ors-radio.co.tz/wp-content/uploads/2024/12/2.jpeg)
Jaji Werema ameacha alama kubwa katika jamii na historia ya nchi, na atakumbukwa kwa mchango wake wa kipekee katika sheria na uongozi. Taarifa kamili kuhusu taratibu za mazishi zitatolewa baadaye.
#RIPJajiWerema
#MwanasheriaMkuuMstaafu