
Shirika lisilo la kiserikali la KINNAPA Tanzania, limefanikiwa kurejesha zaidi ya wanafunzi 200, hasa wasichana, mashuleni katika wilaya za Simanjiro, Kiteto, Babati, Siha na Hai, kupitia mradi wake wa “Mpe Nafasi”.
Katika kikao maalum na waandishi wa habari kilichofanyika hivi karibuni mjini Babati, mkurugenzi Akilimali amesema mafanikio haya yametokana na jitihada za pamoja kati ya shirika hilo, serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

“Kwanza kabisa tangu kuanza mradi huu wa ‘Mpe Nafasi’, tumerejesha watoto zaidi ya 200 shuleni, tumefungua na kujenga uwezo katika klabu zaidi ya 20 za wanafunzi, na tumeelimisha viongozi wa mila na dini pamoja na maafisa elimu katika wilaya zote tano,” alisema Akilimali.
Aidha, Afisa Elimu Wilaya ya Babati, Judith Materu, alisema pamoja na mafanikio hayo, bado changamoto za mimba za utotoni na ukosefu wa mahitaji muhimu zinawafanya wasichana wengi kushindwa kurejea au kubaki mashuleni.
“Kwa mwaka huu pekee, wanafunzi 21 wamerejea mashuleni hapa Babati, wasichana 10 na wavulana 11. Tunafanya kazi kwa karibu na wazazi ili kuhakikisha wasichana wanapata msaada wanaohitaji na jamii inaelewa umuhimu wa elimu,” alisema Materu.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, January Bikuba, alisisitiza kuwa juhudi za pamoja zimefanikisha kupungua kwa visa vya ukatili wa kijinsia kutoka visa 330 mwaka 2022 hadi visa 293 mwaka 2024, huku visa 56 tu vikiripotiwa kuanzia Januari hadi Juni 2025.
“Kuna changamoto za unyanyapaa na hofu ya kulipiziwa kisasi, lakini tumeongeza huduma za msaada wa kisheria na madawati ya jinsia ili kusaidia waathirika,” aliongeza Bikuba.

Kwa upande wake, Mathias Focus, Afisa Ustawi wa Jamii, alitaja ukatili wa kiuchumi na kesi kumalizwa kifamilia kuwa changamoto zinazozuia juhudi za kukomesha kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
KINNAPA imewataka waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kuendelea kusambaza taarifa kuhusu waraka wa elimu namba 2 wa mwaka 2021 na muongozo wa Februari 2022, unaosisitiza kurejeshwa shule kwa watoto wote walioacha masomo, hasa wasichana.